Matokeo ya utafiti huo ulioratibiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF yametolewa leo kuelekea siku ya mtoto duniani tarehe 20 mwezi huu wa Novemba ambapo watoto na vijana wanaamini kuwa maisha ya utoto yamekuwa bora kuliko ya wazazi wao sambamba na huduma za afya na elimu.
Watoto na vijana pia wanajiona wao kuwa raia wa dunia na wanakumbatia ushirikiano wa kimataifa zaidi kukabili changamoto hizo ikiwemo janga la Corona au COVID-19, na wana imani kubwa na wanasayansi katika kutatua changamoto za dunia.
Lakini licha ya matumaini yao, vijana hawajabweteka na kila uchao wanahaha kusaka majawabu ya changamoto zinazokumba dunia hivi sasa ikiwemo madhara ya tabianchi, msongo wa mawazo na kutokuaminika kwa taarifa ambazo wanazisoma kupitia mitandao ya kijamii.
Akizungumzia matokeo ya utafiti huo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema ”kuna sababu lukuki za kuwepo kwa shaka na shuku katika dunia ya leo. Mabadiliko ya tabianchi, umaskini, ukosefu wa usawa, ongezeko la kutoaminiana na uzawa. Lakini kuna sababu pia za matumaini; watoto na vijana wanakataa kuitazama dunia kupitia lensi ya macho ya watu wazima.”
Bi. Fore amesema watoto na vijana wamesalia na matumaini na wana mtazamo wa kidunia na wako tayari kufanya dunia kuwa pahala bora. Vijana wa leo wana hofu ya siku za usoni lakini wanajiona kuwa sehemu ya majawabu.
Kura hiyo ya maoni ilipatiwa jina la Mradi wa kubadilika kwa utoto na ni ya kwanza kufanyika ikihusisha vizazi tofauti ikiwa ni kati ya umri wa miaka 15 hadi 24 na kuanzia miaka 40 na kuendelea.
Wahusika walitoka maeneo ya Afrika, Ulaya, Asia, Amerika Kaskazini na ya Kati na wenye vipato tofauti tofauti.../
342/